2015-01-01

Watanzania Wenzangu;

Kama ilivyo ada imefikia siku ya kuuaga mwaka mmoja na kuukaribisha
mwaka mwingine. Leo tunauaga mwaka 2014 na kuukaribisha mwaka mpya wa
2015. Tunamshukuru Muumba wetu mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na
kutuwezesha kuifikia siku ya leo. Kwa ndugu na jamaa zetu ambao
hawakujaliwa kuiona siku ya leo tuzidi kuwaombea mapumziko mema. Nasi
tumuombe Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema atujaalie umri mrefu, afya
njema na mafanikio tele kwa kila tuliombalo katika mwaka 2015 na miaka
ijayo.

Ndugu wananchi;

Hizi ni salamu zangu za mwisho za mwaka mpya kutoa nikiwa Rais wa nchi
yetu. Mwakani salamu kama hizi zitatolewa na Rais wetu mpya. Mimi
wakati huo nitakuwa raia wa kawaida kijijini kwangu Msoga nikifuatilia
kwenye TV na radio hotuba ya Rais wa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi
yetu akitoa salamu zake za kwanza za mwaka mpya, itakuwa siku ya furaha
na faraja kubwa kwangu.

Hali ya Usalama

Ndugu Wananchi;

Tunaumaliza mwaka 2014 kwa salama na amani. Mipaka yetu iko salama na
hakuna tishio lolote la kiusalama kutoka ndani au nje ya nchi yetu.
Uhusiano wetu na nchi jirani na nyinginezo duniani ni mzuri. Hakuna
nchi iliyo adui au tunayoitilia shaka kuwa na njama za kuhatarisha
usalama wa Tanzania. Nawapongeza wanadiplomasia wetu pamoja na viongozi
na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kuifanya
nchi yetu kuwa salama.

Uhalifu Unapungua

Ndugu Wananchi;

Taarifa za Polisi zinaonyesha kuwa, mwaka 2014 vitendo vya uhalifu
vimepungua ikilinganishwa na mwaka 2013. Mwaka huu, matukio ya uhalifu
yaliyoripotiwa Polisi yalikuwa 64,088 ikilinganishwa na matukio 66,906
katika mwaka 2013. Haya ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la
Polisi wakishirikiana na vyombo vingine vya usalama pamoja na raia
wema. Naomba ushirikiano huu uendelee mwaka ujao na miaka ijayo ili
tuweze kupata mafanikio makubwa zaidi.

Ajali za Barabarani

Ndugu Wananchi;

Nimefarijika kusikia

pia

kuwa matukio ya ajali za barabarani nchini nayo yanaendelea kupungua.
Mwaka huu kumetokea ajali 14,048 zilizosababisha vifo vya watu 3,534 na
wengine 16,166 kujeruhiwa. Mwaka 2013 kulitokea ajali 22,383
zilizosababisha vifo 3,746 na majeruhi 19,433. Hivyo mwaka huu kulikuwa
na ajali 8,335, vifo 212 na majeruhi 3,267 pungufu kuliko mwaka jana.
Huu ni mwelekeo mzuri na wa kutia moyo ingawa bado ni nyingi mno. Naomba
yale tuliyoyafanya yaliyotuwezesha kupata unafuu huu mwaka huu
yaendelezwe maradufu mwaka 2015 na miaka ijayo.
Ugaidi

Ndugu Wananchi;

Mwaka huu tumefanikiwa kutambua mtandao wa viongozi na washirika wao
wanaotuhumiwa kupanga na kufanya mashambulizi ya kigaidi kwa kutumia
mabomu na kumwagia watu tindikali Tanzania Bara na Zanzibar. Watu 112
wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi wametiwa nguvuni.
Tayari watuhumiwa 87 kati yao wameshafikishwa mahakamani na waliosalia
watafikishwa wakati wo wote. Uchunguzi unaendelea ili kuwatambua
wahusika wengine ambao hawajakamatwa.

Ndugu wananchi;

Kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote, natoa pongezi nyingi kwa
vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri waliyofanya ya
kutambua mtandao wa ugaidi nchini na kuchukua hatua thabiti za
kuudhibiti. Hali kadhalika nawashukuru raia wema waliotoa taarifa
zilizowezesha haya kufanyika. Hatupaswi kubweteka wala kudhani kuwa
mambo yamekwisha. Lazima tuendelee kuchukua tahadhari muda wote kwani
hatujui adui anapanga kufanya hujuma gani, lini na wapi.

Dawa za Kulevya

Ndugu Wananchi;

Tumeendelea kupata mafanikio ya kutia moyo katika vita dhidi ya
biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini. Mwaka huu watuhumiwa 935
wakiwemo vigogo wa biashara hii haramu duniani wamekamatwa. Jumla ya
kesi 19 zimefunguliwa Mahakamani. Aidha, kiasi cha kilo 400 za
heroine, kilo 45 za cocaine na kilo 81,318 za bangi zimekamatwa.
Narudia kutoa pongezi nyingi kwa Kikosi Kazi Maalum cha Kukabiliana na
dawa za kulevya nchini kwa mafanikio yanayoendelea kupatikana. Matunda
ya kazi yao tunayaona. Naomba juhudi ziongezwe maradufu mwaka ujao na
miaka ijayo. Serikali itaendelea kuwaunga mkono.

Ndugu wananchi;

Kama nilivyoahidi mwaka jana, Muswada wa Sheria ya Kuthibiti na
Kupambana na Dawa za Kulevya umeshasomwa kwa mara ya kwanza katika
Mkutano wa Novemba, 2014 wa Bunge letu tukufu. Pamoja na kupendekeza
kuongeza adhabu kwa makosa ya kujihusisha na dawa za kulevya, Muswada
huo pia unapendekeza kuanzisha chombo kipya chenye nguvu cha kuzuia na
kupambana na dawa za kulevya. Muswada huu ukipitishwa na kuwa Sheria
tutakuwa tumeongeza nguvu ya mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya
dawa za kulevya nchini.

Ujangili wa Wanyamapori

Ndugu Wananchi;

Katika mwaka tunaomaliza leo mapambano dhidi ya ujangili na biashara
haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori yameimarishwa. Kwa ujumla
kasi ya ujangili imeendelea kupungua. Katika mwaka 2014 ndovu 114
waliuawa ikilinganishwa na ndovu 219 waliouawa mwaka 2013 au ndovu 473
mwaka 2012. Aidha, majangili 1,354 wamekamatwa na pembe za ndovu 542
na silaha mbalimbali 184 nazo zilikamatwa. Naamini uamuzi wa kuifanya
Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa Wakala
yaani Tanzania Wildlife Agency (TAWA) kutaongeza nguvu ya kuhifadhi
wanyama pori na mapambano dhidi ya ujangili.

Natoa pongezi nyingi kwa askari wa wanyamapori, Jeshi la Polisi na
vyombo vingine vya Serikali na raia wema kwa kazi nzuri wanayoendelea
kufanya na mafanikio yanayoendelea kupatikana. Juhudi za kupambana na
ujangili na biashara haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori
zitaendelezwa kwa nguvu zaidi mwaka ujao 2015 na miaka inayofuatia.
Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati marafiki zetu wa
maendeleo wanaotuunga mkono kwa hali na mali katika mapambano haya.
Naomba waendelee kutusaidia.

Hali ya Uchumi Jumla

Ndugu wananchi;

Mwaka 2014 ulikuwa mzuri kwa uchumi wa taifa. Uzalishaji katika sekta
nyingi ulikuwa ni mzuri. Ndiyo maana tunategemea kuwa tutafikia au hata
kuvuka lengo tulilojiwekea la pato la taifa kukua kwa asilimia 7.4 mwaka
huu. Mwaka 2013 pato la taifa lilikua kwa asilimia 7.3. Mfumuko wa
bei uliendelea kushuka na kufikia asilimia 5.8 Novemba, 2014
ukilinganisha na Januari 2014 ulipokuwa asilimia 6.0. Hali nzuri ya
upatikanaji wa chakula nchini imesaidia sana kufanya mfumuko wa bei
kuendelea kushuka. Ni matumaini yangu kuwa mfumuko wa bei utaendelea
kushuka na kufikia asilimia 5 ifikapo Juni, 2015.

Mauzo Nje

Ndugu Wananchi;

Mauzo nje yameendelea kuongezeka. Katika kipindi kilichoishia Oktoba 31,
2014, Tanzania iliuza nje bidhaa na huduma zenye thamani ya dola za
Marekani milioni 8,503.9 ukilinganisha na mauzo ya dola milioni 8,332.5
katika kipindi kama hicho mwaka 2013. Mapato yetu yangekuwa makubwa
zaidi kama bei za kahawa, chai, korosho na pamba zisingeanguka au bei ya
dhahabu nayo isingepada.

Akiba ya Fedha za Kigeni

Ndugu Wananchi;

Akiba yetu ya fedha za kigeni ilikuwa Dola za Marekani milioni 4,251.8
kwa kipindi kilichoishia Novemba 30, 2014. Kiasi hicho kinatuwezesha
kuagiza bidhaa toka nje kwa miezi 4.1. Hii ni chini ya lengo letu la
kuwa na akiba ya fedha za kigeni ya kuagiza bidhaa kwa miezi minne na
nusu. Hata hivyo, sina wasiwasi kabisa kwamba tofauti hii ndogo
tutaweza kuiziba mwaka 2015.

Mapato ya Serikali

Ndugu Wananchi;

Makusanyo ya mapato ya Serikali kwa mwezi, kati ya Julai hadi Novemba,
2014 yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 3,555.5 kipindi kama hicho
mwaka 2013 hadi shilingi bilioni 3,924.1 mwaka huu. Hata hivyo,
makusanyo hayo yalikuwa asilimia 90 ya lengo tulilojiwekea la kukusanya
shilingi bilioni 4,459.7. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato, zipo sababu
mbalimbali zilizosababisha lengo lisifikiwe katika nusu ya kwanza ya
mwaka wa fedha wa 2014/2015. Hatua zipasazo zinaendelea kuchukuliwa
kurekebisha mambo hayo ili katika nusu ya pili ya mwaka huu wa fedha
makusanyo yafikie lengo na ikiwezekana yazidi ili kufidia pengo la nusu
ya kwanza.

Takwimu Mpya za Pato la Taifa

Ndugu wananchi,

Ni utaratibu wa kawaida wa nchi zote duniani kuwa na mwaka unaotumika
kuwa kizio (base year) cha kukokotoa takwimu za Pato la Taifa. Ni
utaratibu wa kawaida pia kwa kila baada ya muda fulani mwaka wa kizio
hubadilishwa. Lengo ni kuboresha takwimu husika. Katika marekebisho
hayo pia huingizwa thamani ya bidhaa na huduma mpya katika pato la taifa
na kuziondoa zilizotoweka ili kutoa picha halisi ya ukuaji wa shughuli
za kiuchumi.

Katika miaka ya hivi karibuni nchi za Ghana (mwaka 2010), Nigeria
(mwaka 2013) na Kenya (mwaka 2014) wamefanya marekebisho ya takwimu zao
za pato la taifa. Na sisi Tanzania tumefanya hivyo mwaka huu (2014).
Hii ni mara ya tano kwa nchi yetu kurekebisha takwimu za pato la taifa.
Mara nne zilizopita ilikuwa mwaka 1966, 1976, 1992 na 2001.

Ndugu wananchi;

Ofisi ya Taifa ya Takwimu imekamilisha marekebisho ya takwimu za pato
la taifa na kukokotoa takwimu mpya kwa kutumia mwaka 2007 kama mwaka wa
kizio. Kutokana na marekebisho yaliyofanyika, pato la taifa kwa mwaka
2013 ni shilingi trilioni 70 kwa kutumia bei za mwaka 2007. Ukitumia
bei za mwaka 2001, pato la taifa kwa mwaka 2013 ni shilingi trilioni
53.17. Kuongezeka kwa pato la taifa kumeongeza pia pato la wastani la
kila Mtanzania kutoka shilingi 1,186,200 (sawa na US$ 742) kwa bei za
mwaka 2001 hadi shilingi 1,560,050 (sawa na US$ 977) kwa bei za mwaka
2007.

Kilimo na Chakula

Ndugu Wananchi;

Mwaka 2014 ulikuwa mzuri sana kwa uzalishaji wa mazao ya chakula nchini.
Uzalishaji ulikuwa tani milioni 16.02 ukilinganisha na uzalishaji wa
tani milioni 14.38 mwaka wa jana 2013. Hili ni ongezeko la tani milioni
1.64. Kwa mujibu wa mahitaji yetu ya chakula nchini kuna ziada ya tani
milioni 3.25. Katika ziada hiyo, mahindi yanachangia tani milioni
1.55, mchele tani 794,000 na kiasi kinachobakia kinachangiwa na mazao
mengine ya chakula.

Ndugu wananchi;

Kuna jambo moja muhimu kuhusu ununuzi wa nafaka ambalo ningependa
kulifafanua. Naomba ieleweke kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula
(NFRA) sio mnunuzi wa mahindi yote, mpunga wote na mtama wote
unaozalishwa na wakulima nchini. Wakala hununua sehemu ndogo tu ya
nafaka ya ziada iliyozalishwa na hununua kwa ajili ya kuweka akiba ya
taifa ya chakula cha kutumika wakati wa dharura ya watu kupata tatizo la
njaa. Aidha, Wakala hununua kiasi kinacholingana na uwezo wa maghala
yake kuhifadhi. Kwa sasa uwezo wa maghala yetu ni kuhifadhi tani 246,000
ingawaje tunaendelea kujenga maghala mengine mpaka tufikie uwezo wa
kuhifadhi tani 400,000 ifikapo 2015. Hivyo basi kwa Wakala kununua tani
292,415.41 mwaka huu ina maana kwamba kiasi cha karibu tani 50,000
zinahifadhiwa nje ya maghala kwa kutumia maturubai. Huu siyo utaratibu
mzuri na haifai kuendelea nao kwani kuna hatari ya nafaka hiyo
kuharibika na kuzua mgogoro mkubwa siku moja.

Ndugu wananchi;

Baada ya NFRA kununua tani 292,415.41 kuna takribani tani milioni 2.96
za nafaka ya ziada ambayo iliyobaki mikononi mwa wakulima. Mategemeo
yetu ni kuwa wafanyabiashara wetu watanunua nafaka hiyo kwa ajili ya
kuuza mijini na kwingineko inakohitajika. Bahati mbaya mwaka huu kama
ilivyokuwa mwaka wa jana, wafanyabiashara wetu hawakuweza kununua
nafaka yote ya ziada ambayo Serikali haikuweza kununua kupitia Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Hali hii imezua tatizo ambalo Serikali kwa
kushirikiana na wafanyabiashara nchini hatuna budi kulitafutia
majawabu. Tunalazimika kutafuta masoko mengine ndani na hata nje ya
nchi ya kuuza mahindi, mpunga na mtama wa ziada. Nimeagiza Wizara ya
Kilimo, Chakula na Ushirika na Wizara ya Viwanda na Biashara kukaa chini
na kushirikiana na wafanyabiashara kulitafutia ufumbuzi suala hili
lenye maslahi makubwa kwa wakulima na nchi yetu kwa jumla.

Ndugu Wananchi;

Katika mazingira haya, ninapopata taarifa ya kuwepo watu wanaotaka
kuuza mahindi nje ya nchi lakini wanawekewa vikwazo na maafisa wa
Serikali inanishangaza na kunisikitisha. Nawataka wale wote wanaofanya
hivyo waache mara moja na badala yake wawasaidie wafanyabiashara hao
kufanikisha azma yao. Hali kadhalika, tuwashawishi watu wengine nao
wajitokeze kufanya biashara hiyo. Jambo muhimu ninalopenda
kulisisitiza ni kwamba pawepo na utaratibu mzuri ili biashara hiyo
ifanywe kwa kutumia njia halali na zilizo wazi. Kutumia njia za panya
hakukubaliki na wala hakuna sababu ya kufanya hivyo.

Miradi ya Kimkakati

Ndugu wananchi;

Katika mwaka 2014 utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kwa mujibu
wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) umeendelea
vizuri. Tunayo matumaini makubwa kwamba katika mwaka 2015 miradi mingi
itakamilika.

Tuanze na Mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara na Songosongo
hadi Dar es Salaam. Mradi huu unategemewa kukamilika Januari, 2015.
Utakapokamilika utatuwezesha kutimiza lengo letu la kuzalisha MW 2,780
za umeme ifikapo 2016. Mipango ya kupata ardhi ya ujenzi wa mitambo ya
kuchakata gesi asili kuwa ya kumiminika (LNG) ili iweze kusafirishwa
kwenda kwenye masoko, inakwenda vizuri.

Ndugu Wananchi;

Utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimkakati wa kusambaza umeme vijijini
umeendelea vizuri na tumepata mafanikio makubwa yasiyokuwa na mfano
wake katika historia ya nchi yetu. Hadi kufikia Novemba, 2014, jumla ya
vijiji 3,836 vimepatiwa umeme na vingine 1,500 vinategemewa kupatiwa
umeme ifikapo Juni, 2015. Hivyo basi, vijiji 5,336 kati ya vijiji
12,423 vya Tanzania Bara vitakuwa vimepatiwa umeme. Hii ni sawa na
asilimia 43 ya vijiji vyote nchini vitavyokuwa vimepata umeme. Hivi
sasa wananchi milioni 17.3 nchi nzima sawa asilimia 36 wamefikiwa na
huduma ya umeme ikilinganishwa na watu milioni 8.1 sawa na asilimia 18.4
waliokuwa wamefikiwa na huduma hiyo mwaka 2012. Mwaka 2015 tunatarajia
watu milioni 18.2 sawa na asilimia 38 watafikiwa na umeme. Kwa upande
wa vijijini mwaka 2012 watu milioni 2.3 sawa na asilimia 7 walikuwa na
umeme. Ifikapo Juni 2015, idadi hiyo itaongezeka na kuwa milioni 7.4
sawa na asilimia 21. Haya ni mafanikio makubwa kwa wananchi wengi
vijijini na mijini kupata umeme katika kipindi kifupi kiasi hiki. Ni
mageuzi ya aina yake yatokayotoa mchango muhimu katika kuinua hali za
maisha ya Watanzania.

Ndugu Wananchi;

Tunaanza kuiona nuru ya matumaini kwamba siku si nyingi kutoka sasa,
makaa ya mawe ya Mchuchuma na madini ya chuma ya Liganga yataweza
kutumika kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wa Ludewa. Maandalizi yote
muhimu yamekamilika kwa ajili ya Januari, 2015 kuanza ujenzi wa mgodi wa
makaa ya mawe kule Mchuchuma, mtambo wa kufua umeme, ujenzi wa mgodi wa
chuma kisichoyeyushwa pale Liganga na ujenzi wa kiwanda cha kuyeyusha
chuma.

Natoa pongezi maalum kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na wabia
wenzao, Kampuni ya Sichuan Hongda ya China kwa hatua iliyofikiwa.
Inakadiriwa kuwa miradi hii ikikamilika itatoa ajira 33,000 za moja kwa
moja na zisizokuwa za moja kwa moja.

Ndugu Wananchi;

Mradi mwingine mkubwa wa kimkakati ni ule wa kujenga Eneo Maalumu la
Kiuchumi (Special Economic Zone) la Mbegani, Bagamoyo. Kwa mujibu wa
mpango kazi wa wabia wa mradi huo yaani Mamlaka ya Kuendeleza Maeneo
huru ya Uwekezaji (EPZA), Kampuni ya China Merchants Holdings
International na Mfuko wa Uhifadhi wa Akiba ya Mali za Serikali ya Oman
(Oman State General Reserve Fund), ujenzi wa bandari na miundombinu
mingine itakayowezesha viwanda kujengwa imepangwa kuanza Julai 2015.

Miundombinu ya Usafiri na Uchukuzi

Ndugu Wananchi;

Katika mwaka huu wa 2014 kazi ya kujenga barabara za lami na kuimarisha
barabara za udongo ili ziweze kupitika wakati wote ziliendelea kote
nchini. Huu nao ni mradi mkubwa wa kimkakati. Barabara za lami 19
zenye urefu wa kilometa 1,459 zimekamilika kujengwa mwaka huu katika
Mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Rukwa, Kagera, Dar es Salaam, Dodoma, Tanga,
Morogoro, Arusha, Tabora na Shinyanga. Ujenzi unaendelea kwa barabara
nyingine 24 katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Kilimanjaro, Rukwa,
Simiyu, Katavi, Tabora, Mwanza, Dar es Salaam, Kagera na Pwani ambazo
wakati wo wote mwaka 2015 zitakamilika. Maandalizi ya kuanza ujenzi wa
barabara nyingine nane yanaendelea vizuri sehemu mbalimbali nchini.

Kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara, tumeendelea kufanya kazi ya
ujenzi na ukarabati wa barabara za udongo kote nchini. Mwaka huu Mfuko
huo umetengewa shilingi bilioni 751.7 ukilinganisha na shilingi bilioni
504.4 mwaka jana. Aidha, mwaka huu tumeweka jiwe la msingi la ujenzi wa
Daraja la Mto Kilombero. Matumini yetu ni kuwa ujenzi wa daraja hilo na
Daraja la Kigamboni utakamilika mwaka 2015. Ujenzi wa Daraja la
Malagarasi ulishakamilika mwaka jana, kinachosubiriwa ni sherehe ya
uzinduzi.

Kwa upande wa jiji la Dar es Salaam, tunategemea kukamilisha ujenzi wa
Awamu ya Kwanza ya barabara za mabasi yaendayo kasi. Ni matarajio yetu
pia kwamba mabasi yataanza kusafirisha abiria katika kipindi cha nusu ya
kwanza ya mwaka 2015. Halikadhalika, tunategemea katika mwaka 2015
ujenzi utaanza wa barabara zinazozunguka jiji la Dar es Salaam (ring
roads), barabara ya Mwenge - Morocco na ile ipitayo juu ya nyingine
(flyovers) eneo la TAZARA. Vile vile, daraja jipya la Salenda litaanza
kujengwa. Aidha, kivuko cha abiria 300 cha MV Dar es Salaam kitaanza
kusafirisha abiria kati ya Dar es Salaam Kaskazini na Ferry mapema
mwakani. Hatua zote hizi zinalenga kupunguza msongamano wa magari
katika jiji la Dar es Salaam.

Usafiri wa Anga na Reli

Ndugu wananchi;

Jitihada za kuboresha huduma ya usafiri katika Reli ya Kati zimeendelea
kwa mafanikio. Mwaka huu vichwa vinane vya treni vimekarabatiwa,
mabehewa mapya 22 ya abiria na mabehewa 274 ya mzigo yamenunuliwa.
Mabehewa hayo yameanza kuwasili nchini kati ya Novemba na Desemba mwaka
huu. Kati ya Januari na Mei, 2015 tunatarajia kupokea vichwa vipya vya
treni 13. Uboreshaji huu wa huduma za treni unakwenda sambamba na
ukarabati wa reli yenyewe, ujenzi wa madaraja na kuimarisha maeneo
yaliyo korofi katika reli hiyo.

Kuhusu ujenzi wa reli iliyo pana zaidi (standard guage), yenye uwezo
wa kubeba mabehewa mengi na kuwezesha treni kwenda kwa mwendo wa kasi
zaidi, juhudi za kutafuta fedha za ujenzi au wabia wa kushirikiana nasi
kujenga zinaendelea. Wakati huo huo, tunaendelea na juhudi za kutafuta
ufumbuzi kwa matatizo ya reli ya TAZARA ili mambo yaende vizuri.
Tutashirikiana kwa karibu na wabia wenzetu wa Zambia. Bahati nzuri
Serikali ya China iko tayari kuunga mkono juhudi zetu za kufufua reli
ya TAZARA.

Usafiri wa Anga

Ndugu Wananchi;

Sekta ya usafiri wa anga imeendelea kukua katika mwaka 2014. Idadi ya
abiria wanaowasili na kutoka katika viwanja vyetu vya ndege nchini
imeongezeka kutoka abiria milioni 2.5 mwaka 2013 hadi abiria milioni
3.5 kufikia Septemba, 2014. Safari za ndege kati ya Tanzania na nchi za
nje zimeongezeka kutoka 274 Januari, 2013 hadi 295 kufikia Septemba,
2014. Hili ni ongezeko la asilimia 8. Safari za ndege ndani ya nchi
nazo zimeongezeka kutoka safari 230,458 mwaka 2013 hadi safari 241,922
mwaka 2014. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 39. Maongezeko haya ni
kielelezo na ushahidi kuwa shughuli za utalii na biashara nchini
zimeendelea kukua.

Ndugu Wananchi;

Ujenzi wa Jengo la 3 (Terminal 3) la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere unaendelea vizuri. Jengo hilo
litakapokamilika mwakani, litakuwa na uwezo wa kuhudumia wastani wa
abiria milioni 8 kwa mwaka. Aidha, ukarabati wa Jengo la 2 (Terminal 2)
utafanyika ili liweze kutoa huduma iliyo bora zaidi. Sambamba na ujenzi
huo, Wakala wa Viwanja vya Ndege wameendelea kukarabati na kuboresha
viwanja vya ndege vya KIA, Mwanza, Songwe, Bukoba, Tabora na Kigoma.
Tunatarajia ukarabati wa viwanja vya ndege vya Shinyanga na Sumbawanga
kuanza mapema mwaka 2015.

Elimu

Ndugu wananchi;

Tumeendelea kupiga hatua za kuridhisha katika kuboresha elimu nchini.
Tumefanikiwa kupunguza tatizo la upungufu wa maabara, vitabu na walimu
wa shule za msingi na sekondari. Mwaka huu tumeajiri walimu 36,339 kati
ya 81,562 wanaohitajika. Tumebakiwa na upungufu wa walimu 45,223 yaani
26,946 wa shule za msingi na 18,277 wa shule za sekondari hususan wa
masomo ya sayansi. Hivi sasa hatuna tatizo la walimu wa masomo ya sanaa
katika shule za sekondari.

Mwaka huu tumeanza mpango maalumu wa kutoa mafunzo ya Diploma ya Ualimu
kwa masomo ya sayansi na hisabati katika Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo
jumla ya wanafunzi 5,602 wa masomo hayo wamedahiliwa. Mpango huu
utatuwezesha kupunguza pengo kubwa tulilonalo la walimu wa sayansi
katika muda mfupi zaidi.

Ujenzi wa Maabara

Ndugu wananchi;

Ujenzi wa maabara za Fizikia, Kemia na Baiolojia katika shule za
sekondari za Kata 3,463 umekwenda vizuri kiasi. Kwa idadi hiyo ya shule
inatakiwa zijengwe maabara 10,389 ilipofika Novemba, 2014. Taarifa
kutoka TAMISEMI zinaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba 29, 2014, maabara
4,207 sawa na asilimia 40.5 zilikuwa zimekamilika, maabara 5,688 sawa na
asilimia 54.8 zilikuwa katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji, na
maabara 494 sawa na asilimia 4. zilikuwa katika hatua za awali za
ujenzi.

Ndugu Wananchi;

Natoa pongezi nyingi kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti na
Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Miji nchini pamoja na
wananchi, kwa jitihada kubwa iliyofanyika. Kwa kutambua jitihada hizo,
nimeongeza miezi sita zaidi kwa wale ambao hawajakamilisha ujenzi wa
maabara hizo wafanye hivyo. Sikusudii kuongeza tena muda baada ya hapo.
Naomba watumie kipindi hicho kitumike kutafuta vifaa vya maabara.
Serikali itasaidia upatikanaji wa watunza maabara (laboratory
technicians) ambao tumeanza programu kubwa ya mafunzo yao na mahitaji
mengine ya maabara.

Ununuzi wa Vitabu

Ndugu Wananchi;

Tumeendelea kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu na vifaa vya
kufundishia katika shule za msingi na sekondari. Tumekuwa tunanunua
vitabu kwa kutumia Bajeti ya Serikali na misaada kutoka kwa marafiki
zetu wa maendeleo. Kwa mfano, Serikali ya Marekani imetupatia vitabu
milioni 2.5 vya masomo ya sayansi na hisabati kwa shule za sekondari.
Ongezeko hili la vitabu linashusha uwiano uliopo sasa wa kitabu kimoja
kwa wanafunzi wanne na kufikia kitabu kimoja kwa wanafunzi wawili. Lengo
letu ni kila mtoto kuwa na kitabu chake kwa kila somo ifikapo mwaka
2016.

Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo

Ndugu wananchi;

Mafanikio mengine tuliyopata mwaka huu ni kukamilika kwa Sera ya Elimu
na Mafunzo ya mwaka 2014. Hii ni hatua muhimu sana katika maendeleo ya
elimu nchini hakuna badala yake. Sera mpya inalenga kuinua ubora wa
elimu na mafunzo na kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha Watanzania
wengi zaidi kupata fursa za elimu iliyo bora na inayolinga na wakati
tulionao. Jambo jipya sana na la kihistoria katika Sera mpya ya Elimu
ni dhamira ya Serikali ya kuondoa ada katika elimu ya sekondari kuanzia
mwaka 2016. Mpaka sasa hatuna ada kwenye shule za msingi, sasa wakati
umefika kufanya hivyo pia kwa elimu ya sekondari. Kwa mujibu wa maelezo
hayo ya Sera, nimekwishatoa maagizo kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Fedha
na Tume ya Mipango kuanza kutafakari namna jambo hilo
litakavyotekelezwa.

Afya

Ndugu Wananchi;

Katika mwaka 2014 jitihada za kuboresha huduma ya afya kwa Watanzania
ziliendelea. Tulipambana kwa mafanikio na mlipuko wa homa ya dengue
iliyowapata watu 1,039 na kusababisha vifo vya watu 3 kati yao. Kwa
upande wa maradhi ya ebola tumejiandaa vya kutosha kutambua watu wenye
maradhi hayo wanapoingia nchini kupitia viwanja vya ndege vya kimataifa
na vituo vyote vya mpakani. Aidha, tumejipanga vyema kuwahudumia
wagonjwa wa maradhi hayo iwapo watatokea.

Mwaka huu pia, Madaktari wetu watano wamekwenda Liberia kusaidiana na
ndugu zetu wa huko katika kukabiliana na ugonjwa wa ebola. Madaktari
wetu hao wako salama na wanaendelea vizuri kutoa huduma. Madaktari hao
watakaporejea nchini watakuwa hazina kubwa ya taifa katika kupanga
mipango ya kukabiliana na ugonjwa huu hatari. Hali kadhalika, watakuwa
viongozi wa wengine katika kutibu wagonjwa wa maradhi ya ebola iwapo
watatokea nchini.

Ndugu Wananchi;

Katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2014, tumeweza kuajiri
watumishi wa sekta ya afya 8,345 ambao kati yao kuna madaktari 244,
madaktari bingwa 75, wauguzi 2,555 na wataalamu wa kada nyingine za afya
5,471. Mwaka huu pia tumefanikiwa kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka
wanafunzi 7,956 katika mwaka 2012/2013 hadi wanafunzi 9,730. Kwa
ongezeko hilo, sasa tumefikia asilimia 97 ya lengo letu la kudahili
wanafunzi 10,000 ifikapo mwaka 2017.

Jitihada zetu za kuongeza fursa za mafunzo kwa Madaktari, Wauguzi na
wataalamu wengine wa afya zina muelekeo mzuri. Ujenzi wa hospitali ya
kufundishia pale Mloganzila unaendelea vizuri na hospitali ya
kufundishia ya Chuo Kikuu cha Dodoma umekamilika. Ni matarajio yangu
kuwa wakati wo wote mwakani ujenzi wa kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha
Muhimbili pale Mloganzila utaanza. Ujenzi huo ukikamilika Chuo kikuu cha
Muhimbili kitaweza kudahili wanafunzi 12,000 kutoka wanafunzi 2,500 wa
sasa jambo ambalo litafanya upungufu wa Madaktari, Wauguzi na Wataalamu
wa Afya kupata jawabu la uhakika. Tumeendelea kufanya mambo mengine
ikiwemo ujenzi wa jengo la tiba za ubongo na mishipa ambalo limekamilika
pale Muhimbili, sasa tunahangaikia kupata vifaa.

Maji

Ndugu Wananchi;

Katika mwaka huu wa 2014 tumeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya
kuwapatia wananchi maji safi na salama mijini na vijijini. Kwa ajili
hiyo miradi 498 ya maji vijijini imekamilika na miradi 740 ipo katika
hatua mbalimbali za ujenzi. Miradi mingine 378 ipo katika maandalizi ya
ujenzi kuanza. Ni matarajio yetu kwamba katika mwaka ujao wa 2015,
miradi mingine 731 itatekelezwa na vituo 25,790 vya kuchota maji
vitajengwa. Miradi hii ikikamilika tutaweza kuwafikia asilimia 71 ya
wananchi wanaopata maji safi na salama vijijini kutoka asilimia 58 ya
sasa. Kwa ajili hiyo, tutakuwa tumevuka lengo tulilojiwekea la kuwapatia
watu maji asilimia 65 ya Watanzania waishio vijijini ifikapo 2015. Ombi
langu kwa ndugu zetu wa Hazina waiangalie sekta hii ya maji kwa ukaribu
zaidi na wawapatie fedha kwa wakati.

Ndugu Wananchi;

Utekelezaji wa mradi wa kuipatia maji miji ya Mwanga – Same – Mkomazi
pamoja na miji na vijiji vyote vya njiani, utaanza Februari, 2015.
Fedha zimekwishapatikana na Mkandarasi wa Awamu ya Kwanza
ameshapatikana. Makandarasi wa Awamu ya Pili na Tatu watapatikana muda
si mrefu kutoka sasa. Hii pia itahusu kupata Mkandarasi wa mradi wa
maji wa mji wa Orkesment.

Ndugu Wananchi;

Mwaka huu miradi ya kuipatia maji miji kadhaa nchini ilikamilika na
tatizo la upungufu wa maji litakuwa limepatiwa ufumbuzi. Ipo miji
kadhaa ambayo miradi imefikia hatua ya juu na kwamba wakati wowote
mwakani itakamilika. Jiji la Dar es Salaam lipo katika kundi hili.
Kazi ya upanuzi wa miradi ya maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini kwa msaada
wa Serikali ya Marekani na mkopo kutoka Serikali ya India imefikia hatua
nzuri. Inatarajiwa kukamilika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2015.
Mwaka ujao pia visima virefu vya Kimbiji na Kipera vitachimbwa na Bwawa
la Kidunda litaanza kujengwa.

Serikali ya India pia imekubali kutupatia mkopo wa Dola za Marekani
milioni 268.2 kwa ajili ya kugharamia mradi wa kuipatia maji miji ya
Tabora, Nzega na Igunga kutoka Ziwa Victoria. Uwezekano wa kujumuisha
miji ya Sikonge na Urambo katika mradi huo utaangaliwa.

Bunge na Mahakama

Ndugu Wananchi;

Katika mwaka 2014, mihimili ya Bunge na Mahakama iliendelea kutekeleza
vyema majukumu yao. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeweza
kuendesha shughuli zake kama ilivyopangwa pamoja na kulazimika kugawana
Ukumbi ule wa Bunge na Bunge Maalum la Katiba. Bunge limefanya mikutano
mitatu, Miswada 17 ya Sheria ilisomwa kwa mara ya kwanza, Sheria tano
na maazimio saba yalipitishwa. Maswali ya msingi 569 na ya nyongeza
1,541yaliulizwa na kujibiwa. Aidha, sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow
nalo lilijadiliwa na kutolewa maazimio. Tumeshaanza kuchukua hatua
kuhusu maazimio hayo na bado tunaendelea.

Napenda kuitumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Wabunge wetu kwa
kutekeleza vizuri wajibu wao wa Kutunga Sheria na kusimamia Serikali.
Nawasihi waendelee na msimamo huo mwema na chanya kwa maslahi ya nchi
yetu na watu wake.

Ndugu Wananchi;

Kwa upande wa Mahakama napenda kutambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa
ya kupunguza mrundikano wa mashauri katika Mahakama za ngazi zote.
Wahenga wamesema “mcheza kwao hutunzwa”. Hatuna budi kutoa pongezi
maalum kwa Jaji Mkuu, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman kwa uongozi wake
mahiri. Chini ya uongozi wake Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa
Mahakama Kuu na Mahakimu Wakazi na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo
wamejiwekea malengo ya kusikiliza na kutoa hukumu kwa mashauri
yasiyopungua 200 kwa mwaka kila mmoja wao.

Habari njema na ya kuleta faraja ni kwamba utekelezaji unaendelea
vizuri. Mashauri 870 yalisikilizwa na kuamuliwa kwenye Mahakama ya
Rufani, mashauri 11,334 kwenye Mahakama Kuu, mashauri 8,715 kwenye
Mahakama ya Mahakimu Wakazi na Mashauri 25,683 katika Mahakama za
Wilaya. Aidha, mkakati wa kupeleka timu ya Majaji wa Mahakama Kuu kwa
wakati mmoja kwenye maeneo yenye mashauri mengi kama ilivyofanyika
Kigoma, Shinyanga na Tabora umesaidia sana kupunguza mrundikano wa
mashauri ya siku nyingi. Haijawahi kutokea mashauri mengi kiasi hicho
kusikilizwa na kumalizwa katika historia ya Mahakama nchini.

Ndugu Wananchi;

Mkakati huu mpya umeleta matumaini mapya kwamba tatizo la kuchelewesha
kwa mashauri ambalo lilidhaniwa kuwa ni tatizo sugu sasa limeanza
kupatiwa ufumbuzi. Kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote natoa shukrani
na pongezi nyingi kwa Jaji Mkuu, Majaji wa Rufani, Jaji Kiongozi,
Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakimu wa ngazi zote kwa kazi nzuri
waifanyayo.

Hali kadhalika, nampongeza Mtendaji Mkuu wa Mahakama na watendaji wote
wa Mahakama kwa kazi nzuri waifanyayo ya kuwawezesha Majaji na Mahakimu
kutimiza ipasavyo majukumu yao. Hakika utendaji Mahakamani umebadilika
na kuwa bora zaidi. Mimi naahidi kuendelea kusaidia Mahakama kwa
kuwahimiza ndugu zetu wa Hazina kutoa kwa wakati pesa zilizotengwa
katika bajeti.

Mapambano Dhidi ya Rushwa

Ndugu Wananchi;

Mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka yameendelea
bila ya ajizi. Katika mwaka huu wa 2014 TAKUKURU wamepokea taarifa 237
na wamekamilisha uchunguzi wa mashauri 545. Watuhumiwa waliofikishwa
Mahakamani ni 428. Mashauri yaliyomalizika ni 205, kati ya hayo 125
watuhumiwa waliachiliwa na 80 walipatikana na hatia na kuhukumiwa.
Mwaka huu wa 2014 mali na fedha taslimu zenye thamani ya shilingi
bilioni 38.96 zimeokolewa. Katika kuimarisha Taasisi hiyo kiutendaji,
maafisa wapya 394 wameajiriwa.

Sherehe za Miaka 50 ya Muungano

Ndugu Wananchi;

Mwaka huu wa 2014 tuliadhimisha miaka 50 ya Muungano wa nchi zetu mbili
yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika kwa heshima
inayostahili. Maadhimisho yalifikia kilele tarehe 26 Aprili, 2014 na
zilifanyika sherehe nchini kote na sherehe hizo zilifana sana. Ni
ukweli usiopingika kuwa kwa Muungano wetu kuweza kudumu kwa nusu karne
ukiwa bado imara na unazidi kustawi ni mafanikio makubwa. Matumaini kwa
siku za usoni ni mazuri. Naamini Muungano wetu utaimarika zaidi iwapo
Katiba Inayopendekezwa itapitishwa kwani yale mambo yenye kuleta
matatizo hivi sasa yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi.

Miaka 50 ya JWTZ

Ndugu Wananchi;

Wakati nchi inasherehekea miaka 50 ya Muungano, baadhi ya vyombo na
taasisi muhimu kitaifa zilifanya hivyo hivyo. Miongoni mwa
walioadhimisha nusu karne ya kuundwa kwake ni Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania kama mjuavyo JWTZ ilizaliwa tarehe 1 Septemba,
1964. Jeshi letu liliadhimisha siku yao hiyo kwa kufanya zoezi kubwa la
kivita lililoanza Kibaha mkoani Pwani na kumalizikia Monduli Mkoani
Arusha.

Nilibahatika kushuhudia siku ya mwisho ya zoezi hilo. Nilifurahishwa
sana na kiwango cha utayari kivita cha Jeshi letu. Wanajeshi wetu
walionesha weledi wa hali ya juu, umahiri mkubwa, ujasiri, ukakamavu na
uvumilivu wa aina yake wakati wa kutekeleza majukumu yao katika
mazingira magumu ya uwanja wa medani za vita. Niliwapongeza siku ile na
narudia tena leo kuwapongeza. Niliyoyaona yamenihakikishia mimi na
Watanzania wote kuwa Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania liko
imara kulinda mipaka ya nchi yetu na kuhakikisha usalama wa taifa letu
na watu wake. Jeshi letu bado ni lile tunalolijua sisi sote, lakini
limezidi lile lililomng’oa mvamizi Dikteta Iddi Amin wa Uganda, tena
limezidi kwa mbali.

Mchakato wa Katiba Mpya

Ndugu Wananchi;

Mwaka huu pia tumeshuhudia kukamilika kwa zoezi muhimu la kuandika
Katiba Inayopendekezwa. Kama tujuavyo sote, mchakato uliozaa Katiba
Inayopendekezwa ulikuwa na changamoto nyingi ndani na nje ya Bunge
Maalum la Katiba. Pamoja na hayo, Bunge hilo lilikamilisha kazi yake kwa
salama siku mbili kabla ya tarehe 4 Oktoba, 2014 ambayo ndiyo ilikuwa
siku ya mwisho. Mimi na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed
Shein tulikabidhiwa nakala za Katiba Inayopendekezwa tarehe 8 Oktoba,
2014. Nimeshatimiza wajibu wangu wa kuchapisha katika Gazeti la
Serikali na kutangaza siku ya kupiga kura ya maoni kuwa tarehe 30
Aprili, 2015. Nimeshatoa maagizo kwa Tume ya Uchaguzi kufanya
matayarisho husika ya kuwezesha Kura ya Maoni kufanyika.

Ndugu Wananchi;

Moja ya mambo muhimu ambayo Tume ya Uchaguzi inafanya kwa sasa ni
kuandikisha wapiga kura katika Daftari la Mpiga Kura. Tume imeamua
kutumia mfumo mpya wa Biometric Voters Register. Uandikishaji wa
majaribio umefanyika katika baadhi ya Kata katika Majimbo ya Mlele, Kawe
na Kilombero. Matatizo yaliyojitokeza yatasaidia kuboresha mfumo huo
kabla ya uandikishaji wa watu wote wenye sifa stahiki kuanza.

Ndugu Wananchi;

Napenda kutumia nafasi hii kuwafahamisha Watanzania wenzangu wote kuwa
mfumo mpya unatengeneza Daftari Jipya la Mpiga Kura ingawaje lugha
inayotumika ni uboreshaji wa Daftari la sasa. Uboreshaji huu wa Daftari
la Mpiga Kura ni tofauti na ule tuliouzoea ambapo walikuwa
wanaandikishwa wapiga kura wapya na wale waliopoteza vitambulisho vyao.
Safari hii wanaandikishwa wote wapya na wa zamani na wote watapata
vitambulisho vipya. Hivyo basi, sisi wenye vitambulisho vya kupiga kura
vya zamani tusifanye ajizi, tujitokeze kujiandikisha wakati ukifika.

Jambo la pili ni kwamba, Daftari la Mpiga Kura linalotayarishwa siyo kwa
ajili ya Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa peke yake, daftari
hilo hilo litatumika pia kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015. Hivyo
basi, kujiandikisha ni jambo muhimu sana. Usipofanya hivyo siyo tu
utajinyima fursa ya kushiriki kuamua kuhusu Katiba Inayopendekezwa bali
pia utakosa fursa ya kuchagua Rais wako, Mbunge wako na Diwani wako.
Katu usikubali yakukose hayo.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Ndugu Wananchi;

Kama mjuavyo tarehe 14 Desemba, 2014 na 20 Desemba, 2014 ulifanyika
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuchagua viongozi wa vitongoji, vijiji na
mitaa. Uchaguzi umekwisha na viongozi wamekwishapatikana. Sasa ni
wajibu wa viongozi hao kufanya kazi waliyoiomba. Kwa walioendesha
uchaguzi ni wakati mzuri wa kufanya tathmini ili wapate mafunzo
yatokanayo na uchaguzi huo. Kwa TAMISEMI na Wakurugenzi Watendaji wa
Halmashauri, lengo liwe ni kuona namna ya kuimarisha mazuri na
kusahihisha makosa na matatizo yaliyojitokeza. Kwa walinzi wa amani
watambue matatizo ya kiusalama yaliyotokea na kuona namna ya kutengeneza
mikakati ya kuzuia matatizo ya namna hiyo yasijitokeze tena. Hatma ya
yote, shabaha yetu ni kutaka kufanya vizuri zaidi katika chaguzi zijazo
za Serikali za Mitaa na kufanya vizuri zaidi katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015.

Jumuiya ya Afrika Mashariki

Ndugu Wananchi;

Mwaka huu Tanzania imechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Ni zamu yetu kwa mujibu wa mzunguko wa uongozi wa Jumuiya
yetu kati ya nchi wanachama. Ni dhamana kubwa na kwamba wenzetu wa
Afrika Mashariki wanatutegemea tuwaongoze katika kutekeleza malengo na
madhumuni ya Jumuiya kama yalivyoainishwa katika Mkataba ulioanzisha
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hali kadhalika, tunategemewa kuongoza
katika utekelezaji wa maamuzi mbalimbali ya vikao vya Jumuiya. Hii
inahusu maamuzi yaliyokwishafanywa kabla yetu ambayo utekelezaji wake
unaendelea na uamuzi mpya utakaofanywa katika kipindi cha uongozi wetu.

Kwa niaba ya Watanzania wote napenda kuwashukuru ndugu zetu wa Burundi,
Kenya, Rwanda na Uganda kwa kutuamini. Napenda kuahidi kuwa
hatutawaangusha. Sisi Watanzania tutafanya kila tuwezalo kuimarisha
Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa manufaa ya Jumuiya yenyewe, nchi zetu na
wananchi wa Afrika Mashariki. Tutajitahidi kuwa wabunifu kwa nia ya
kuona utangamano unakua na kustawi kwa kasi na kuzaa matunda ya
maendeleo tunayoyatarajia sote. Matunda tuliyoyatarajia tulipoamua
kuanzisha Jumuiya hii na matunda tuliyoyapata tulipoamua kwa hiari yetu
kujiunga nayo kuwa wanachama.

SADC, AU NA UN

Ndugu Wananchi;

Kuhusu Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika
na Umoja wa Mataifa, tunaahidi kuendelea kuwa wanachama waaminifu na
kushiriki kwa ukamilifu katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za
mashirika haya ya kikanda na kimataifa. Kwa upande wa SADC tutaendelea
kushiriki katika utekelezaji wa mikakati na mipango ya maendeleo ya
kiuchumi na kijamii na ile ya kisiasa na kiusalama kama ilivyoainishwa
katika RISDP (Regional Indicative Strategic Development Plan) na SIPO
(SADC Strategic Indicative Plan for the Organ). Kwa ajili hiyo Tanzania,
itaendelea kutoa mchango wake katika kukuza utangamano wa kiuchumi
katika SADC na kusaidia kuimarisha uhusiano mwema na usalama miongoni
mwa nchi wanachama wa SADC. Hii ni pamoja na kusaidia katika kutatua
migogoro ya kisiasa na kusalama kati ya nchi wanachama.

Kwa upande wa Umoja wa Afrika tutaendelea kutekeleza maamuzi ya vikao na
taasisi mbalimbali za Umoja huo. Daima tutakuwa wanachama waaminifu wa
Umoja wa Afrika na kuchangia katika uimarishaji wake. Kuhusu Umoja wa
Mataifa tutaendelea kutimiza wajibu wetu kama wanachama wa Umoja huo wa
kimataifa ulio adhimu na muhimu kwetu na dunia nzima. Tutaendelea
kushiriki katika shughuli za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa.
Hivi sasa tunao wanajeshi wetu katika majeshi ya kulinda amani ya Umoja
wa Mataifa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Sudan na
Lebanon. Tuko tayari wakati wote kuchangia zaidi iwapo Umoja wa Mataifa
watatutaka tufanye hivyo.

Hitimisho

Ndugu Wananchi;

Namaliza hotuba yangu hii ndefu kwa kuwashukuru Watanzania wote kwa
kuiunga mkono Serikali yetu na kwa mchango wenu uliowezesha nchi yetu
kupata mafanikio haya makubwa tunayojivunia katika mwaka 2014. Tumeweza
kuvuka mitihani na nyakati zenye majaribu mengi. Umoja wetu na
mshikamano wetu ndivyo vilivyotuwezesha kufika hapa. Tunauanza mwaka
2015 kwa matumaini makubwa. Mwaka 2015 unatupa fursa kubwa ya kuendelea
kuliimarisha zaidi taifa letu. Mwaka ujao ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu,
hivyo huenda ukawa na changamoto na majaribu magumu zaidi kuliko mwaka
huu. Uelewa wetu, umoja wetu, mshikamano wetu na moyo wetu wa uzalendo
ndivyo vitakavyotuvusha kama ilivyokuwa kwa miaka ya nyuma. Mimi nina
imani kubwa kwa uwezo na utayari wa Watanzania wenzangu kuidumisha sifa
nzuri ya nchi yetu ya umoja na mshikamano wa watu wake uliozaa amani na
utulivu. Tumeweza mwaka huu na miaka ya nyuma, tutaweza tena mwakani na
miaka ijayo. Inawezekana, Timiza Wajibu Wako! Nawatakia heri ya mwaka
mpya.

Mungu Ibariki Afrika!

Mungu Ibariki Tanzania!

Asanteni kwa kunisikiliza.

Show more